Dar es Salaam. Licha ya ujumbe wa Rais wa Marekani, Barrack Obama kutarajiwa kufikia katika hoteli kubwa zenye hadhi wakati kiongozi huyo atakapowasili nchini Julai Mosi mwaka huu, Ikulu ya Marekani imetoa tahadhari ya vyakula ambavyo hawatakiwi kuvigusa wakiwa nchini ikiwa ni pamoja na kutumia maji ya bomba.
Mbali na tahadhari hiyo, ziara hiyo ya Obama itakuwa na ulinzi mkubwa
ambao pengine haujawahi kutokea katika historia ya viongozi wa nje
wanaotembelea Tanzania kwani utahusisha idadi kubwa ya magari, ndege za
kijeshi na meli kubwa ya kivita ambazo zitakuwa zikifanya doria karibu
na pwani ya Tanzania.
Tahadhari za matumizi ya chakula, maji na nyinginezo zimetolewa
katika nchi zote tatu za Afrika ambazo Obama atatembelea, kila moja kwa
jinsi Wamarekani hao wanavyoitathmini.
Rais Obama atatembelea nchi za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Vyombo vya usalama vya Marekani vimejipanga kuhakikisha ziara ya
kiongozi huyo haivurugwi kwa namna yoyote ile. Tayari ndege za jeshi
zilizobeba magari ya akiba 56, yakiwemo 14 aina ya ‘Cadillac One’
maalumu kwa ajili ya kiongozi huyo, yamewasili katika nchi hizo tatu za
Afrika atakazotembelea.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post la Marekani, ndege hizo pia
zimebeba malori matatu ambayo yamesheheni karatasi maalumu za kuzuia
risasi kupenya kwenye vioo, zitakazobandikwa kwenye madirisha ya hoteli
ambazo Rais Obama na ujumbe wake watafikia.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mamia ya mashushushu wa Marekani tayari
wako katika nchi hizo. Meli maalumu za kubeba ndege za kivita, maarufu
kwa jina la ‘amphibious ship,’ ikiwa na hospitali maalumu na yenye vifaa
vyote itaweka nanga baharini, jirani na nchi atakayokuwa Rais Obama,
tayari kukabiliana na dharura yoyote itakayotokea. Gazeti hilo
liliandika kuwa ndege za kivita za Marekani zitakuwa zikipeana zamu
kufanya doria kwa saa 24, katika anga la nchi ambayo Rais Obama
atakuwepo, iwapo ndege za ‘adui’ zitakaribia eneo linaloitwa ‘anga ya
rais.’ Kwa mujibu wa gazeti hilo, ziara ya Rais Obama aliyoifanya hivi
karibuni katika nchi za Ujerumani na Ireland Kaskazini, japo kulikuwa na
gharama kwa walinzi, lakini safari za nchi za Afrika zimeelezwa kuwa na
gharama kubwa zaidi.
Tahadhari
Kwa mujibu wa taarifa ya maelekezo ya Ikulu ya Marekani, ambayo
Mwananchi imepata nakala yake, watu watakaokuwa kwenye msafara wa Obama
wametakiwa kutotumia kachumbari. Pia imewataka kutumia maji ya chupa
zaidi.
“Kutokana na mfumo wa maji uliopo, tunashauri watu wetu kutumia maji
ya chupa zaidi kwa kunywa na hata kwa kupiga mswaki,” ilisema taarifa
hiyo.
Kwa kuelewa fika tatizo la ugonjwa wa malaria nchini, ujumbe wa Obama
umeshauriwa kutumia dawa ya mbu ya kupaka na kupuliza inayoitwa Deet.
Deet ni dawa maarufu huko Marekani na ikiwa katika aina tofauti ikiwamo ya kupaka na kupuliza na imekuwa ikitumiwa na jeshi la Marekani kwenye vita mbalimbali tangu miaka ya 1940 kabla ya kuanza kutumiwa na raia mwaka 1957.
Deet ni dawa maarufu huko Marekani na ikiwa katika aina tofauti ikiwamo ya kupaka na kupuliza na imekuwa ikitumiwa na jeshi la Marekani kwenye vita mbalimbali tangu miaka ya 1940 kabla ya kuanza kutumiwa na raia mwaka 1957.
ATM nazo noma
Pia watu watakaokuwa kwenye msafara wa Rais Obama wametakiwa
kuhakikisha wanatumia mashine za kutolea fedha (ATM) zilizoko karibu na
hoteli watakazofikia.
“Kuna tatizo la uhalifu kwa hiyo siyo vizuri kutumia ATM ambazo ziko
katika sehemu zisizo salama. Pia katika kipindi watakachokuwa Tanzania
watu wanapaswa kutumia teksi ambazo zimeidhinishwa na hoteli.
“Pia siyo vizuri kuacha kompyuta ya fedha kwenye vyumba mtakavyolala.
Pia kina mama wanapaswa kuchukua tahadhari ya mabegi yao watakapokuwa
wanapita mitaani,” ilitahadharisha taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment