DAR ES SALAAM, Baada
ya miaka 10 ya ‘ndoa’ kati ya kipa Juma Kaseja na Simba ya Dar es
Salaam, klabu hiyo ya jezi nyekundu na nyeupe kutoka Mtaa wa Msimbazi
imetangaza rasmi kuachana naye.
Kaseja
alisajiliwa Simba mwaka 2003 akitoka klabu ya Moro United, na tangu
wakati huo alikuwa kipa tegemeo wa Simba kwa misimu tisa akiiwezesha
kutwaa mataji kadhaa ya Ligi Kuu.
Katika
kipindi chote cha kucheza Simba, Kaseja ambaye pia ni nahodha wa Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), ni mara moja tu mwaka 2009 alijiunga
na mahasimu wakubwa wa Simba, Yanga na kucheza msimu mmoja.
Uamuzi
wa kuachana na Kaseja ulifikiwa na Kikao cha Kamati ya Ufundi
kilichoketi juzi na jana na kuamua kutoendelea naye tena baada ya
mkataba wake kumalizika.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Danny Manembe alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa,
klabu yao ina makipa watatu wapya, hivyo hawana tena sababu ya kuendelea
na Kaseja.
Makipa
waliopo Simba kwa sasa ni Abel Thaira, Andrew Ntala aliyesajiliwa
kutoka Kagera Sugar na Abuu Magube aliyepandishwa kutoka kikosi B.
“Tuna
makipa watatu, hawa ni wengi sana kwetu. Hatuwezi tena kuongeza kipa
mwingine, hivyo Kaseja tunaachana naye,” alisema Manembe. Akiongeza,
Manembe alisema kocha mpya wa Simba, Abdallah Kibadeni katika orodha ya
wachezaji anaowataka kwa ajili ya msimu ujao, hakumjumuisha Kaseja hivyo
na wao wameamua kuachana naye.
Muda
mfupi kabla ya Simba kutangaza uamuzi huo, Mwananchi iliwasiliana na
Kaseja ambaye alisema: “Sitaki kuzungumzia habari za Simba kwa sasa,
nina mambo mengi muhimu nataka kuyafanya.”
Itakuwa
mara ya kwanza kwa Simba kuanza msimu wa ligi bila Kaseja kwa miaka
tisa, huku kipa huyo pia akiweka rekodi ya kucheza mechi nyingi za
watani, ambapo mpaka anatemwa ameshasimama longoni mechi 25.
No comments:
Post a Comment