Friday, 14 June 2013

TCU YAPIGA STOP TIU KUTOA SHAHADA

images

Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) imekifunga Chuo Kikuu cha Kimataifa Tanzania(Tanzania International University -TIU) kudahili wanafunzi  ngazi ya shahada kutokana na  kutotimiza masharti na vigezo vinavyohitajika na Tume hiyo ili kuendesha mafunzo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa habari mwandamizi wa Tume hiyo Edward Makaku,  (leo) jijini Dar es salaam amesema kuwa Chuo hicho kimefungwa kutokana na kutotimiza masharti ya kufundisha kozi ya shahada ikiwa ni pamoja na kukosa walimu wanaokidhi vigezo vya kufundisha ngazi hiyo.
 “Tunapenda kuwatangazia kuwa chuo hicho ni chuo kikuu binafsi na kimesajiliwa kuendesha mafunzo yake kwa leseni namba CR1/028 na imepitiwa na Tume ya vyuo vikuu na kuruhusiwa kutoa mafunzo yake kwa ngazi ya cheti, stashahada na kozi za muda mfupi lakini sio kwa ngazi ya shahada, naomba wananchi waelewe hili”, alisema Edward.
Aidha  Edward ameongeza kuwa mapema Aprili mwaka huu Tume ilitoa mwongozo kukitaka chuo hicho kusitisha  mafunzo yake katika ngazi ya shahada mpaka kitakapokidhi masharti na kupatiwa usajili.
“Napenda kutoa tahadhari kwa wananchi kutojiunga na chuo hicho kwa ngazi ya shahada kwani hakijakidhi vigezo vya kutoa shahada kama inavyotakiwa na Tume bali wanaweza kujiunga katika ngazi za cheti, stashahada na mafunzo ya muda mfupi”, ameongeza.
 Tume imeutaka uongozi wa  chuo hicho kuacha kudahili wanafunzi na kurudisha ada na gharama nyinginezo kwa walosajiliwa ngazi ya shahada.

No comments:

Post a Comment