- Wadau wengi wanataka Simba ibadilishe uamuzi wa kumtema Juma Kaseja kwa vile bado ana uwezo mkubwa na ndiyo maana ni nahodha wa Taifa Stars.
Kwa wiki nzima sasa, suala la Kaseje kutemwa
limekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari, huku ikielezwa kuwa uamuzi huo
umewagawa viongozi wa klabu, kwani baadhi yao wanataka aendelee kubaki.
Rafiki wa karibu wa Kaseje amelitonya gazeti hili
jana kuwa, kipa huyo kwa sasa yuko nje ya jiji na kwamba anatarajia
kuzungumza kwa mara ya kwanza kuhusu hatima yake Simba Jumapili wiki
hii.
Mwenyekiti wa Simba na hata kocha Abdallah
Kibadeni walikaririwa wakisema, kipa huyo aliyesajiliwa mwaka 2003
kutoka Moro United hatakuwamo kwenye kikosi hicho msimu ujao.
Kipa wa zamani wa klabu hiyo, Moses Mkandawile
ameshutumu uamuzi wa Simba kumtema Kaseja kwani, yeye binafsi anaamini
Kaseja ndiye kipa bora kwa sasa Tanzania.
“Huyu ni nahodha wa timu ya Taifa, ikiwa na maana
kwamba kiwango chake bado kiko juu. Sasa iweje Simba wamteme kwa madai
ya kushuka kiwango? Kweli uamuzi huu unashangaza sana,” alisema
Mkandawile.
“Nadhani kuna chuki binafsi kati yake na baadhi ya
viongozi ndiyo maana wengine wanapinga Kaseja kutemwa,” alisema zaidi
kipa huyo wa zamani.
Aidha, Katibu Mkuu wa zamani TFF, Fred Mwakalebela
naye alishangazwa na uamuzi wa Simba kumtema kipa huyo na kusema
haukuzingatia uwezo wake, bali chuki kutoka kwa baadhi ya viongozi wake.
Mwakalebela alisema, anaamini Kaseja bado ni kipa
mwenye uwezo wa kucheza timu yoyote kwa vile kiwango chake bado kinadai
tofauti na mawazo ya watu wengine.
Kwa upande wake, mchezaji wa zamani Yanga Kitwana
Manara alisema walichokifanya kwa Kaseja siyo sahihi hata kama mpira
umekwisha anatakiwa apewe heshima yake kama mchezaji aliyeitumikia klabu
muda mrefu.
“Huyu ni alama ya mafanikio Simba, alipaswa kupewa
heshima kubwa. Kama hawataki kumsajili, basi wangemweka kwenye benchi
la ufundi,” alisema Manara.
Kwa upande wake, nyota wa zamani Taifa Stars,
Peter Tino alisema masuala ya usajili waachiwe viongozi na benchi la
ufundi na kwamba wasisikilize kelele za mashabiki.
No comments:
Post a Comment