Maandalizi ya ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama nchini yanazidi kupamba moto huku maofisa wa usalama wa Marekani wakipiga kambi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Aidha, kutokana na ujio huo, Serikali imeagiza mashirika yote ya ndege kubadili ratiba zao za safari Julai Mosi, siku ambayo Rais huo atatua nchini.
Jana, waandishi wetu walishuhudia pilikapilika za kuimarisha ulinzi katika uwanja huo jambo ambalo uongozi wa uwanja huo jambo wamelieleza kwamba halijawahi kutokea.
Ulinzi haujawahi kutokea
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Moses Malaki alisema jana kwamba ratiba za uwanjani hapo
zitabadilika kutokana na uzito wa ugeni huo.
Alisema kwa kawaida anapokuja kiongozi mkubwa wa kitaifa katika uwanja huo hakuna ndege inayoruhusiwa kutua kwa kipindi cha nusu saa.
“Ni kweli hali hiyo pia itakuwapo atakapokuja Rais Obama na safari za ndege zitabadilika kulingana na ratiba ya kutua na kuondoka kwa Rais huyo,” alisema Malaki.
Pia alisema ulinzi katika uwanja huo umeimarishwa kwa mwezi mmoja sasa na tangu wakati huo, maofisa wa usalama wa Marekani wamekuwa wakifika kwa nyakati mbalimbali.
“Sijawahi kuona ulinzi mkali kama huu, wamekuja marais wengi hapa nchini lakini ulinzi huu ni wa kutisha, sijui kwa sababu gani?” alisema Malaki.
Alisema awali, wakati maofisa hao walipoanza kuwasili nchini hawakutambua ni mgeni gani anayetarajia kufika lakini baadaye walipelekewa taarifa kuwa ni Rais Obama na baadaye walitaarifiwa kuwa angetua saa 8.40 mchana, Julai Mosi.
Mkurugenzi huyo alisema Rais Obama atakuja na ndege nne, moja itakayombeba, ya pili kwa ajili ya mizigo, ya tatu itakuwa ya waandishi wa habari na maofisa wa usalama na ya mwisho ni kwa ajili ya dharura ambayo itaegeshwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Malaki alisema maofisa wa Marekani wanaowasili nchini wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kuhakikisha kuwa hali ya usalama inaimarishwa na kuwaacha wazawa wakifanya shughuli za kawaida.
“Ulinzi ni mkali mno, yapo masharti kadhaa wanayoyataja kuwa
yatatumika kwa watu watakaoingia eneo la uwanja au kuisogelea ndege ya
Rais Obama. Jamaa wameweka masharti magumu,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema maofisa hao wanakuja kwa makundi na hivi karibuni lilifika kundi la kusimamia mawasiliano ambayo yatatumiwa wakati watakapokuwa nchini.
“Pia wamechukua kwa muda karakana ya Shirika la
Ndege la Precision Air iliyoko kwenye eneo la Uwanja wa Ndege. Maofisa
wa Usalama wa Marekani wanataka kufanya shughuli ndani mle,” alisema
Malaki.
Pia, ndege mbovu zilizokuwa kwenye maeneo ya
uwanja huo zimeondolewa. Viongozi wa Precision Air hawakupatikana
kuzungumzia suala hilo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania
(TCAA), Fadhili Manongi alisema ni utaratibu wa kawaida kwa karakana
kuazimwa wakati wanapokuja wageni mashuhuri.
“Nafasi ile mara nyingi hutumiwa na maofisa wa
usalama pale wanapokuja wageni mashuhuri kwenye Uwanja wa Ndege wa
Julius Nyerere,” alisema.
Alidokeza pia pamoja na ugeni wa Rais Obama, pia
kumekuwa kuna presha ya ugeni wa marais wa nchi mbalimbali duniani
wanaokuja kuhudhuria mkutano wa Smart Partnership unaonza keshokutwa.
Pia wana kazi ya kuwapokea wake za marais wa
Afrika watakaokutana na mke wa Rais Obama, Michelle na mke wa Rais wa
zamani wa nchi hiyo, George Bush, Laura.
Kazi inayofanyika
Ofisa mmoja wa Uwanja Ndege ambaye hakutaka jina
lake litajwe, alisema maofisa hao walifanya ukaguzi wa hali ya juu
kwenye sehemu mbalimbali za uwanja huo wakitumia mitambo maalumu ya
kung’amua mabomu.
“Hawa jamaa wako juu sana katika mambo ya usalama
maana wana kifaa cha kuchunguza mabomu hata yaliyo chini ya ardhi,”
alisema na kuongeza kuwa licha ya kukagua uwanja huo, pia walikwenda
mbali zaidi na kukagua maeneo ya jirani.
Mitambo mbalimbali ya shughuli za usalama imefungwa kwenye eneo hilo la uwanja na maofisa wa Marekani walionekana wakiwa juu ya paa la moja ya majengo ya uwanja huo wakifunga mitambo katika minara mirefu kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano.
Yavuruga ratiba za ndege
Manongi alisema kampuni za ndege zimeagizwa
kufanya mabadiliko ya ratiba za safari siku atakapowasili Rais Obama ili
kutoa nafasi kwa anga hilo kutumika kwa shughuli za mapokezi yake.
Alisema kampuni zote za ndege zimeshapewa taarifa kuhusu hatua hiyo.
“Kubadilishwa kwa ratiba kunatokea mara kwa mara
na huwa tunawapa taarifa kampuni za ndege mapema ili wajue namna ya
kujipanga,” alisema Manongi.
Kutua Senegal leo
Rais Obama anatarajiwa kuanza ziara yake ya barani
Afrika leo na alitarajiwa kutua Dakar, Senegal saa 9.30 alasiri kwa saa
za Afrika Mashariki.
Akiwa nchini humo, ratiba inaonyesha kuwa atakuwa
na mazungumzo na Rais wa Senegal, Macky Sall kwenye Ikulu ya nchi hiyo.
Pia ratiba hiyo inaonyesha kuwa atakutana na majaji kutoka mikoa yote ya
nchi hiyo.
Pia atakwenda katika Kisiwa cha Goree ambacho kiko
kwenye Bahari ya Atlantic na atatembelea Jumba la Makumbusho katika
kisiwa hicho ambacho kilikuwa kituo cha kuhifadhi watumwa waliokuwa
wanasafirishwa kutoka Afrika kwenda Marekani.
“Baada ya shughuli hiyo, Rais Obama atahudhuria
dhifa ya taifa kabla ya kupumzika kwa muda mfupi na kuanza safari ya
kwenda Afrika Kusini,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu ya Marekani.
No comments:
Post a Comment