Saturday, 1 June 2013

YANGA YALETA KATIBU MKUU MPYA KUTOKA KENYA

Yanga yaajiri Katibu Mkuu kutoka Kenya hii mashabiki wa Yanga inawahusu sana story yote hii hapa


Pichani ni Makao Makuu ya timu ya Yanga ya jijini Dar es salaam yaliyopo maeneo ya mtaa wa Jangwani 


MABINGWA wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, Yanga ya Dar es Salaam wameanza mazungumzo na msomi mmoja kutoka Kenya kwa nia ya kumpa nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo yenye makazi yake katika makutano ya mtaa wa Jangwani na Twiga.
Mwanaspoti linajua kwamba mchakato huo unaendelea kwa siri sana jijini Dar es Salaam na Yanga sasa inataka kujiendesha kiprofesheno zaidi ndio maana imeamua kuchukua mtaalamu wa kigeni na mwenye uwezo mkubwa.
Habari za ndani kutoka mtaa wa Jangwani zinasema msomi huyo raia wa Kenya ana elimu nzuri ya utawala na kuwapo kwake kutaifanya Yanga kujiendesha kisasa zaidi kama zilivyo klabu za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini au Esperance ya Tunisia.
Habari hizo zinadai kuwa uongozi wa Yanga umefanya hivyo baada ya kutoridhishwa na jinsi mambo ya kiutendaji yanavyofanyika katika klabu hiyo yenye mashabiki wengi nchini.
Hakuna kiongozi yeyote wa Yanga aliyekuwa tayari kuzungumzia hilo, lakini Mwanaspoti linajua kuwa kuna mkakati mkubwa wa mabadiliko unafanywa Jangwani hasa katika nafasi ya Katibu Mkuu.
Kama Yanga itafanikisha mchakato huo itakuwa klabu ya kwanza nchini kuajiri kiongozi wa kigeni. Yanga sasa ipo chini ya Kaimu Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako ambaye alipewa nafasi hiyo kwa muda baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Selestine Mwesigwa kusitishiwa mkataba wake.
Awali Jamal Malinzi na Lucas Kisasa wamewahi kuwa makatibu wakuu wa Yanga kwa vipindi tofauti tangu mwaka 2000.

No comments:

Post a Comment