Tuesday, 2 July 2013

WAKENYA WAMUITA JUMA KASEJA NAIROBI

TIMU mbili nchini Kenya zimejitosa kumuwania kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja ili zimsajili kwa ajili ya msimu ujao.
Wakala wa kuuza wachezaji nchini, John Ndumbaro, amealiambia Championi Jumatatu kuwa, timu hizo mbili zimemtaarifu kuwa zinataka kumsajili Kaseja kwa ajili ya msimu ujao.
“Kuna timu ambazo nisingependa kuzitaja hadi hapo kutakapokuwa na makubaliano kwa kuwa ni suala la Kaseja mwenyewe kukubali au la.
“Mimi nafanya kazi na timu hizo katika masuala ya kuuza wachezaji, sasa zimenieleza nia yao ya kumsajili Kaseja baada ya kusikia amemaliza mkataba wake na Simba na hawajamuongezea.
“Nafikiri mazungumzo yataanza hivi karibuni na kama kutakuwa na mafanikio, basi tunaweza kutangaza ni timu zipi na mambo yamekuwaje. Kwa kifupi hapa ni suala la maslahi na uamuzi wa mwenyewe Kaseja,” alisema Ndumbaro ambaye ni mdogo wa wakala mwingine Damas Ndumbaro.
Kaseja sasa yupo huru baada ya kumaliza mkataba na Simba ambayo imetangaza haitamuongezea mkataba mpya na kumpa ruhusa ya kuendelea na ‘mishe’ zake.
Kaseja yupo mapumzikoni nyumbani kwao Kigoma ambako pia amekuwa akiendelea na mazoezi mepesi na vijana wengine mjini humo. Anatarajiwa kutua Dar leo.
Wakala huyo alisema ndani ya wiki moja anatarajia kuwa amejua uamuzi wa Kaseja na iwapo atakuwa amekubali kujiunga na timu kati ya hizo mbili ambazo zinaendelea kupambana katika Ligi Kuu Kenya.

No comments:

Post a Comment