MBUNGE
wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kujiuzulu ubunge,
ikiwa itabainika anajihusisha biashara ya dawa za kulevya. Kauli hiyo
imekuja siku
chache baada ya kutajwa katika moja ya barua iliyosambazwa
katika mitandao ya kijamii, baada ya mtu anayedaiwa kukamatwa China na
kuwatuhumu watu kadhaa akiwamo Idd Azzan. Akizungumzia kuhusu sakata
hilo jana, alisema hatua ya kuhusishwa na biashara haramu ya dawa za
kulevya, ni kutotenda haki mbele ya jamii hasa wapiga kura wake na Taifa
kwa ujumla. Alisema mtu aliyendika barua ya tuhuma dhidi yake, ni wazi amedhamiria kumshushia heshima na huenda akawa ana jambo limejificha. “Ni
kweli nimeiona hiyo barua katika mtandao, inayodaiwa imeandikwa na
kijana ambaye amekamatwa Hong Kong nchini China. Lakini ninajiuliza kama
kweli yeye ni raia mwema, katika hili kwanini hakutaka kutaja jina lake
kwenye barua hiyo.
“Hata
nilipoisoma nimebaini kuwa huyo mtu ametumika na huenda kabisa hayupo
nje ya nchi, kwani katika maelezo yake anataja jina la Balozi Philip
Marmo kuwa amemsaidia hali ya kuwa hivi karibuni Rais Kikwete alimteua
Balozi mpya Abdulrahman Shimbo na Marmo kuwa Balozi wa Shirikisho la
Ujerumani. “Kingine naona alijaribu kuandika uongo kuweza kuaminisha
jamii, kwani hata hilo jila la balozi mwanzo limetajwa jina la Bernad na
kukatwa kwa wino. Ninapenda kulieleza Taifa kuwa naomba vyombo vya
usalama vifanye uchunguzi wa jambo hili na nikibainika ninauza dawa za
kulevya nipo tayari kujiuzulu ubunge wangu.
“Kubwa
haki itendeke katika kufanya uchunguzi wa jambo hili, ila ni lazima
jamii na Watanzania kwa ujumla tusikubali kwa makusudi watu waichafue
nchi yetu kwa chuki na fitna tu,” alisema Azzan.
Alisema kutokana
na hali hiyo, anashindwa kuchukua hatua yoyote ya kufanya zaidi ya
kuliandikia barua Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi dhidi ya barua hiyo
kuweza kubaini ukweli wa jambo hilo.
“Sijawahi kuuza dawa za
kulevya na hata katika familia yangu hakuna mtu anayefanya biashara hiyo
haramu. Kila mmoja anajua kuwa Idd nilikuwa Diwani wa Kata ya Magomeni,
huku kazi yangu kubwa ikiwa ni biashara ya magari na daladala ambayo
ninaendelea nayo hadi sasa mbali ya ubunge kama nilivyopewa heshima na
wapiga kura wangu wa Kinondoni,” alisema Azzan.
Alipoulizwa kuwa
ni hatua gani ikibainika hakuna ukweli wa jambo hilo baada ya vyombo vya
usalama kufanya uchunguzi, alisema atakachokifanya anamuachia Mungu.
“Ni
ngumu kusema hatua gani nitachukua ikibainika hakuna ukweli, lakini
nataka kusema kama yule aliyeandika barua hii angetaja jina lake ni wazi
baada ya uchunguzi ningeweza kuomba ushauri kwa mwanasheria wangu hatua
za kuchukua, lakini kwa kuwa hakutaja jina ni ngumu kuweza kuamua,”
alisema Azzan.
Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa kupitia mitandao,
ziliripoti kukamatwa kwa Watanzania wawili nchini China wakiwa na dawa
za kulevya zenye thamani ya Dola milioni 3.34 za Marekani.
|
No comments:
Post a Comment