Raia wawili wa Kenya, wamekamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), wakipanda mlima huo bila kuwa na kibali.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete, alisema jana kuwa watu hao walikamatwa na askari wa wanyamapori wa Kinapa na wamekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria.
Aliwataja Wakenya kuwa ni Robert Mwadime Mwakana (30) na Dickson Kawa Mbole (27), ambao walikamatwa Julai 13, mwaka huu.
Alisema Wakenya hao wanaotoka eneo la Taveta nchini Kenya, wanasadikiwa kuingia Hifadhini kwa kupitia vichakani na walikamatwa kati ya eneo la Lango la Marangu na Kituo cha Mandara wakiendelea na safari ya kupanda mlima.
Pia watu watatu wa familia moja wamekamatwa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha wakishirikiana na polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali, ambazo ni mifupa mitatu ya twiga yenye uzito wa kilo 10.4 na mfupa mmoja wa tembo wenye uzito wa kilo tano.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Charles Mollel, Alex Mollel na Samwel Mollel, ambao walikamatwa katika eneo la Kisongo Olasite kufuatia taarifa kutoka kwa raia wema.
Shelutete alisema askari hao walimkamata Elias Sifael, ambaye ni mkazi wa Leguruki Nkoasenga kwa kukutwa na silaha aina ya Shotgun namba C 139415 inayoaminika kutumika kwa ujangili.
Kwa mujibu wa sheria viwango vya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa Mtanzania na raia wa Afrika Mashariki ni Sh. 1,500 kwa siku.
Kwa mujibu wa sheria viwango vya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa Mtanzania na raia wa Afrika Mashariki ni Sh. 1,500 kwa siku.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alithibitisha kukamatwa kwa Wakenya hao na kudai kuwa watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
Alisema Wakenya hao walikuwa wanapanda mlima na vifaa vya kupandia mlima kufanya utalii na pasi za kuingilia nchini na kwamba, hawakukutwa na silaha yoyote.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment