Friday, 5 July 2013

Mke wa Mandela aeleza hadharani hali ya mumewe




Johannesburg. Mke wa Nelson Mandela, Graca Machel kwa mara ya kwanza amejitokeza hadharani kuzungumzia hali ya kiafya ya mumewe kwamba kuna wakati anazidiwa lakini hajambo.
Graca alisema hayo jana kwenye sherehe za uzinduzi wa siku ya Utamaduni na Michezo ya Nelson Mandela iliyofanyika kwenye Kituo cha Kumbukumbu ya Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini.
Alieleza sababu za kuhudhuria sherehe hizo kwamba kubwa ni kuwashukuru kwa kuwa pamoja na kumwombea afya njema Mandela tangu alipolazwa hospitali Juni 8, mwaka huu.
Graca alisema pamoja na kwamba Mandela amelala akiugua hospitali, lakini ameendelea kutoa zawadi kwa wanajamii wote ya kuwaunganisha pamoja, ambayo ni michezo na utamaduni.
“Madiba kuna wakati hayuko vizuri. Wakati mwingine anakuwa na maumivu. Lakini hajambo,” alinukuliwa Graca akizungumza katika sherehe hizo.
Katika hatua nyingine mjini Pretoria, Rais Jacob Zuma juzi alisema kuwa hali ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela bado ni mbaya na hakuna mabadiliko.
Rais Zuma alisema hayo baada ya juzi (Jumatano) jioni kwenda hospitali kumjulia hali Mandela, ambapo alikuwa na msafara mkubwa.
Kiongozi huyo pia aliwaomba wananchi wa Afrika Kusini kutenga dakika 67 kwa ajili ya Siku ya Mandela ya Julai 18, ambayo ni siku yake ya kuzaliwa.
Alisema kauli mbiu ya siku hiyo ni “Chukua hatua; penda mabadiliko; fanya kila siku iwe siku ya Mandela kwa kujielekeza katika masuala ya chakula, makazi na elimu.
Wakati huohuo, kumekuwa na hali ya utulivu katika eneo la Hospitali ya Medi-Clinic aliyolazwa Mandela, tofauti na ilivyozoeleka kuwa na pilikapilika nyingi.
Kwa mujibu wa taarifa, watu wanaopita eneo hilo la hospitali wamekuwa wakionekana wakiwa na hali ya utulivu, huku wengine wakipiga picha kwenye kadi, maua, bendera, vipeperushi na mabango yaliyowekwa kandokando ya hospitali hiyo, yakiwa na ujumbe wa kumtakia nafuu ya kuumwa Madiba.
Wakati hali hiyo ikiendelea kutokea mjukuu wa Mandela, Mandla Mandela ameendelea kuikoroga familia hiyo, baada ya kuzungumza na waandishi wa habari akidai kushangazwa na mahakama ilivyoharakisha kesi hiyo kuhusu mvutano wa sehemu ya kuzikwa Mandela na siyo miaka miwili iliyopita baada ya yeye kufukua makaburi
.

No comments:

Post a Comment