Friday, 19 July 2013

SERIKALI YASISITIZA KUWA "KODI YA LINE ZA SIMU" IKO PALE PALE



Waziri wa Fedha, William Mgimwa, amesisitiza uamuzi wa Serikali kuendelea kutoza Sh 1,000 kwa kila mwezi kwa laini ya simu, licha ya kampuni za simu na wanasiasa kupinga.

Akizungumza na mwandishi juzi, Mgimwa alikumbusha wanaolalamikia kodi hiyo, kwamba suala la ulipaji kodi kwa taasisi au watu binafsi, ni la kisheria kulingana na mapato yao na hali halisi iliyopo.
 

Pia alieleza kushangazwa na matangazo ya baadhi ya kampuni kuhusu utozwaji kodi wananchi akisema wananchi ndio wanataka barabara, maji na umeme vijijini na kodi hizo zinakwenda kutumika huko.


Kwa mujibu wa Mgimwa, kodi ya laini za simu na ya intaneti, imetengwa ikatumike kusaidia maji na uwezo wa Serikali kupeleka elimu vijijini jambo ambalo ni la maendeleo.
 

"Wananchi wenyewe wanalalamikia ukosefu wa huduma na baada ya Serikali kupitia na kufanyia kazi changamoto hizo, imeridhia kodi hizo wanakuja watu wanalalamika," alisema.

 
Alisisitiza kuwa ongezeko la kodi kwa huduma za intaneti, ni kwa ajili ya kuboresha mfumo wa elimu ambao unalalamikiwa mara kwa mara.


Mgimwa alisema ulipaji kodi unatokana na aina ya biashara na mapato na kutaka kampuni zinazokatwa kodi, kutojilinganisha na kampuni zingine.


Alishangaa wabunge wanaolalamikia ulipaji Sh 1,000 za simu, kwa maelezo kwamba kodi hiyo haikupendekezwa na Serikali, bali Bunge kupitia Kamati ya Bunge lilitaka wananchi wakatwe Sh 1,450.


Baada ya mapendekezo, Mgimwa alisema Serikali ilifanya  uchambuzi na kuamua kupunguza hadi Sh 1,000.   

 
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, jana alisema msimamo wa Serikali ndio wake pia.
 

Kauli ya Mgimwa inajibu malalamiko ya baadhi ya kampuni, wabunge na vyama vya siasa, kwamba ongezeko hilo linaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.


Hivi karibuni kampuni za simu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), walilalamikia kodi hiyo kwamba inaongeza gharama za maisha kwa wananchi.


Mbali na Mnyika, hata CCM kupitia taarifa ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilitaka kodi hiyo iondolewe na Serikali itafute vyanzo vingine vya mapato. 


Pia Chama cha Watoa Huduma za Mitandao ya Intaneti Tanzania (TISPA), walilalamikia sheria mpya ya kodi na ushuru wa bidhaa katika intaneti, kwamba itachangia ongezeko la gharama za huduma ya intaneti kwa watumiaji wa kawaida.


No comments:

Post a Comment