Friday 5 July 2013

Abiria 18 wanusurika katika ajali huko Lushoto, Tanga


ABIRIA waliokuwa wakisafiri na basi dogo lijulikanalo kwa jina la Morama lenye namba za usajili T 284 AUH, wakitokea Tanga kwenda Lushoto, Alhamisi ilopita nusura wapinduke chini ya milima ya Usambara, baada ya basi hilo kukwepa fuso wasigongane uso kwa uso. 

Tukio hilo limetokea majira ya saa 4:00 usiku katika kona iliyopo katika kijiji cha Bangala, nusura lisababishe maafa makubwa kwa abiria waliopakiwa kutokana na dereva aliyekuwa akienda basi hilo kukata ghafla kulikwepa fuso lililokuwa limesheheni makabichi kutokea Mlalo. 

Mmoja wa abiria aliyekuwemo kwenye basi hilo, Bw. Shadrack Thobias alisema kabla ya kutokea tukio hilo dereva wao alikuwa akiyumba na kupotexza mwelekeo katika barabara hiyo ndogo nyembamba kulikosababisha na madai kwamba alikuwa amelewa viroba tangu aanze safari ya kupandisha katika milima hiyo. 

"Tulipopita kwenye kizuizi cha polisi eneo la Bangala, askari polisi walitusimamisha wakazungumza na dereva pamoja na kondakta wake, walichukua muda mrefu, tulipoondoka kwenye kizuizi hicho dereva alianza kwenda mwendo wa kasi," alisema Thobias. 

Alisema ghafla walikutana na fuso lililokuwa limebeba makabichi lakini sehemu ya barabara ilikuwa ndogo na walipopishana dereva wa basi ilibidi atoke barabarani lakini kule alipokuwa akikwepa fuso hilo, gari hilo liliserereka na kutaka kutumbukia chini ya milima lakini bahati nzuri difu ya gari iligonga chini ikawa inaning'inia kwenye miti iliyoizuia gari isitumbukie chini. 

"Kwa kweli ni rehema za mungu tu ndizo zimetuokoa vimnginevyo ile gari ingetumbukia chini umbali karibu wa mita 200 kutoka juu ya barabara ni hatari sana lakini tatizo dereva wetu alikuwa aemekunywa viroba," alisema Thobias. 

Waandishi wawili wa habari kutoka Jijini Dar es salaam, ambao hawakutaka majina yao yasitajwe hapa kwa kuwa walikuwa kwenye safari zao za binafsi, walisema kwamba tatizo kubwa lililosababisha ajali hiyo kutokea ni umakini mdogo wa dereva kulikosababishwa na kunywa pombe.

 "Kwa kweli jeshi la polisi linahitajika kufanya kazi zao ipasavyo kwa madereva wanaoonekana kukiuka sheria...Polisi waliokuwa kwenye kizuizi kile kama wangekuwa makini kwenye kazi zao pengine wangemropoa dereva asiendelee na udereva lakini hawakumpima wala kusikia harufu yake ya pombe," alisema mmoja wao ambaye anatangaza televisheni moja kubwa. 

Hata hivyo, Mkuu wa polisi wa wilaya ya Lushoto Bw. Zuberi Madafu alipoulizwa kuhusu kutokea ajali hiyo, alikiri kutokea lakini akasema kwamba basi hilo halikuwa na abiria hata mmoja wakati likipata ajali hiyo hata alipothibitishiwa kuhusu waandishi wa habari wawili kupanda humo bado alitetea kwamba halikuwa na abiria. 

"Ni kweli basi la Morama limepata ajali lakini nilimtuma mkuu wa usalama barabarani amekwenda asubuhi leo (Ijumaa Julai 5) amekutana na wafanyakazi wa basi wamemwambia kwamba hawakuwa na abiria isipokuwa walikuwa wakilijaribu gari lao na walikuwa wakitokea Mombo kuja Lushoto," alisema OCD Madafu na kuongeza; 

"Kama wapo abiria walipanda kwenye basi hilo na wakapata misukosuko hiyo waje kituoni waripoti ili tufungue kesi lakini tumeenda na wamesema hawakuwa na abiria wowote mle ndani,".

basi la Morama likiwa limeziba barabara.
Coaster liitwalo Tende Sheki likipita kwa tabu baada ya Morama kupata ajali eneo hilo
mabasi yakiwa yamesimama.
foleni ya mabasi yanayokwenda Lushoto
wafanyakazi wa Morama wakitafuta njia za kuliondoa gari lao

No comments:

Post a Comment