Saturday, 17 August 2013

KUTEKWA KWA PONDA NI HARAKATI ZA SERIKALI KUWAPENDELEA WAKRISTO"....UJUMBE WA VIPEPERUSHI VINAVYOSAMBAZWA KWA WAISLAMU



SAKATA la Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, limeendelea kuwa gumzo katika maeneo mbalimbali, huku matamko makali yakitolewa dhidi ya Serikali.

Sakata hilo limeonekana kutikisa na kutawala vyombo vya habari, baada ya kiongozi huyo wa dini kudaiwa kupigwa risasi, kusomewa mashtaka kitandani na baadaye kupelekwa gerezani chini ya ulinzi mkali akitolewa katika Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI).

Suala hilo limeibua hisia nyingine baada ya masheikh jijini Dar es Salaam, kutoa tamko lenye mwelekeo wa kupinga udhalilishwaji wa kiongozi huyo na kuionya Serikali juu ya mwenendo huo.

Mbali na masheikh kutoa tamko jana, Jeshi la Polisi kwa upande wake nalo liliimarisha ulinzi katika Msikiti wa Kichangani, uliopo Magomeni na ule wa Mtambani uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba, alisema kitendo hicho ni kibaya kwani kinapandikiza chuki baina ya Waislamu na Serikali.

Sheikh Katimba ambaye alikuwa ameongozana na masheikh kadhaa akiwamo Amiri wa Shura ya Maimamu, Sheikh Musa Kundecha, alitoa tamko hilo katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana.

“Tunalaani kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda, tukio la kupigwa risasi na baadaye kudhalilishwa kwa kuondolewa hospitali wakati akipatiwa matibabu, ni jambo baya linakwenda kinyume na haki za binadamu.

“Tukio hili limeibua hisia kali kwa Waislamu, hivyo tunaitaka Serikali kuacha kuwatesa na kuwadhalilisha viongozi wa dini ya kiislamu, kwani kufanya hivyo ni kupandikiza chuki miongoni mwa Waislamu.

“Waislamu wamekuwa wakiamini kwamba, ufumbuzi wa suala la amani ya kweli na ya kudumu ya nchi ni kuweza kushughulikia madai ya msingi ya Waislamu dhidi ya Serikali ambayo ndio chanzo cha madai ya kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda,” alisema Sheikh Katimba wakati akisoma tamko hilo lililosainiwa na Sheikh Juma Said Ally.

Waitisha mkutano wa dharura kesho

Kutokana na suala hilo, jumuiya hiyo imeitisha mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho katika viwanja vya Nurul Yakin vilivyopo Wilaya Temeke, jijini Dar es Salaam ambapo tamko litatolewa juu ya mustakabali wa suala hilo.

Katika tamko hilo, Sheikh Katimba alisema kuwa hatua hiyo inaweza kuzidisha chuki baina ya Waislamu na vyombo vya dola kwa madai kuwa vimekuwa vikiwakandamiza Waislamu.

“Kitendo cha kumpiga risasi Sheikh Ponda na kisha kumchukua kutoka hospitali na kumpeleka gerezani kwa kukiuka taratibu ni kinyume cha haki za binadamu.

“Matibabu ni haki mojawapo kwa binadamu yeyote hata kama kuna wanaomtuhumu. Tuhuma si sababu ya kukiuka taratibu, kuvunja sheria na hata kumtisha unayemtuhumu, kwani njia hiyo haiwezi kutatua bali inazidisha ukubwa wa tatizo.

“Tunalaani kwa mara nyingine kitendo cha Polisi na Usalama wa Taifa kutenda vitendo vinavyoashiria uonevu kwa viongozi wa dini ya Kiislamu, pia tunaitaka Serikali kutenda uadilifu kwa raia wake hata pale inapoamini kuwa raia hao wana makosa.

Sheikh Basaleh aonya

Kwa upande wake mjumbe wa Taasisi ya Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Alli Basaleh alikemea vikali tukio la kupigwa kwa Sheikh Ponda na kusema kuwa jamii inapaswa kupinga vitendo vya watu kuteswa na kunyanyaswa vinavyofanywa na vyombo vya dola.

“Hii ni ishara ya huko tuendako kwa baadaye, nchi inaweza kuingia kwenye machafuko, ni wazi kabisa hata katika mataifa ambayo amani imevurugika hali ilianza kama hivi kama njia ya kupinga uonevu wa Serikali dhidi ya watu wake.

“Tuwe makini na hali hii hakuna taifa lolote linaloweza kuhubiri amani pasipo kuwa na umoja na masikilizano baina ya viongozi wa Serikali na watu wake,” alisema Sheikh Basaleh.

Polisi waranda misikitini

Hata hivyo wakati viongozi hao wakiendelea na mkutano na waandishi wa habari jana, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika Msikiti wa Mtambani ambapo gari tatu zilikuwa zikiranda nje ya msikiti huo huku zikiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

MTANZANIA iliwashuhudia askari hao wakiwa katika gari aina ya Defender zenye namba za usajili PT 2118 na PT 2083, ambazo zilikuwa nje ya msikiti huo.

Hata hivyo wakati askari wakiwa wanaranda katika eneo hilo la Msikiti, baadhi ya makundi ya Waislamu walikuwa wakigawa vipeperushi vilivyokuwa vimeandaliwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ambavyo vilihoji. “Kwa nini Serikali ya CCM imempiga risasi Sheikh Ponda?”

Mbali na Msikiti wa Mtambani, askari pia walikuwa wametanda katika Msikiti wa Magomeni Kichangani, ambapo anatoka Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Kundecha.

MTANZANIA ilifanikiwa kunasa kipeperushi kilichosomeka kwa maneno yafuatayo; “Kwa nini Serikali ya CCM imempiga risasi Sheikh Ponda, polisi waliotaka kumuua sasa wamemteka kutoka Muhimbili hadi Segerea akiwa bado mgonjwa.

“Hii imefanyika ili mfumo wa kuwakandamiza Waislamu na kuwapendelea Wakristo uweze kudumu na kuweza kupewa fedha na Serikali chini ya Mkataba (MoU),” ilisomeka sehemu ya kipeperushi hicho.

Alipopigwa mkoani Morogoro

Agosti 10, mwaka huu akiwa mkoani Morogoro, Sheikh Ponda, alidaiwa kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni risasi, ambapo Agosti 15, mwaka huu Jeshi la Polisi nchini liliripoti kushikiliwa kwa askari anayedaiwa kufyatua risasi hiyo.

Katika mahojiano aliyofanya na Gazeti la MTANZANIA Agosti 11, mwaka huu, Sheikh Ponda alisema polisi walidhamiria kumuua kwa makusudi ili wapoteze ushahidi. Huku akidai kuwa jeraha lake analodai limetokana na kupigwa risasi.

Sheikh Ponda alieleza kuwa alipigwa risasi na polisi wakati akiwa kwenye gari na wenzake. “ Nilimuona kwa macho yangu askari mmoja ambaye alikua amevaa sare akinilenga kwa mtutu wa bunduki,” alisema Ponda.

Monday, 5 August 2013

OMMY DIMPOZ APIMA HIV NA KUSEMA "SINUNUI WALA KUUZA MECHI TENA"


Hii Ndio Post Yake kwenye Instagram Ya Star Wa Single Mpya 'Tupogo'Ommy Dimpoz Kuhusu Kupima HIV Na Kuamua Kuto Uza au Kununua Mechi Tena.
Kwenye Interview ya simu niliyo fanya nae leo, Ommy ameniambia hizi ndio sababu za yeye kupima H I V 
  1. Kujua Afya ili ujilinde na uwe mtu bora.
  2. Kukinga wengine baada ya kujua afya yako pia ni muhimu.

JAJI FRANCIS MUTUNGI ATEULIWA KUWA MSAJILI MPYA WA VYAMA VYA SIASA...TENDWA KWA HERI

huyu ndio msajili mpya wa vyama vya siasa....................

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji Francis S.K. Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Taarifa iliyotolewa Dar Es Salaam leo, Jumatatu, Agosti 5, 2013, na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza Ijumaa iliyopita Agosti 2, 2013.

Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. John Tendwa ambaye amestaafu Utumishi wa Umma kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, DAR ES SALAAM.

WANYARWANDA WAANZA KUREJEA MAKWAO BAADA YA RAIS KIKWETE KUWAPA SIKU 14 ZA KUONDOKA

story yote iko hapa


Mamia ya wahamiaji haramu kutoka nchini Rwanda wakiwa na ng’ombe zaidi 900 wameanza kuondoka nchini kurejea kwao kutokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete kuwataka waondoke Tanzania kabla ya siku 14. 

Aidha, imeelezwa kuwa kumekuwapo ongezeko la askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mkoani Kagera hasa wilayani Ngara hali inayozua hofu kwa baadhi ya wananchi, huku ikiongeza msukumo kwa wahamiaji haramu kuondoka.

Akiwa katika ziara mkoani Kagera, Rais Kikwete alitoa agizo la kuwataka wote waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria waondoke mapema jambo lililotakiwa kuanza kutekelezwa Julai 29 na kukamilika Agosti 10 mwaka huu.

Alisema kuwa wahamiaji haramu na wale wanaoendesha ama kuhusika na ujambazi, uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua mwafaka za kuondoka mapema kabla vyombo vya ulinzi na usalama kuanza operesheni maalumu ya kuwasaka.

Tayari idadi kubwa ya wafugaji wenye makundi ya ng’ombe imeanza kuondoka kuelekea eneo la mpakani la Rusumo kutoka ardhi ya Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa agizo hilo la Rais Kikwete.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu alisema kwamba idadi kubwa ya wafugaji waliokuwa wakiishi kinyume cha sheria, imeitikia wito wa agizo la Rais na kuanza kuondoka kwa hiyari yao.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na idadi kubwa ya wahamiaji kuanza kuondoka, bado wapo ambao hawajaondoka kutokana na kudai kuwa na vibali walivyovipata kutoka Ofisi ya Uhamiaji na kubainisha kwamba vibali hivyo vitakaguliwa kwa umakini wakati wa operesheni maalumu ili kujua uhalali wake.

“Jambo hili la wahamiaji haramu lilikuwa kero kubwa, siyo tu kwa Wilaya ya Ngara, bali mkoa mzima wa Kagera, lakini tunashukuru sasa wameanza kuondoka, wamebaki hao wenye vibali. Ni lazima vibali hivyo tutavikagua maana vipo vilivyotolewa kinamna,” alieleza Kanyasu.

Alionya kwamba jukumu la kuwaondoa kwa nguvu wahamiaji haramu pamoja na wafugaji linasubiri muda wa mwisho ili kuanza kutekelezwa kama Rais Kikwete alivyoagiza.

Hofu ya Wanajeshi kuongezeka

Akizungumzia suala la wanajeshi kudaiwa kuongezeka wilayani Ngara, Kanyasu alisema kwamba katika wilaya yake kuna kikosi cha dharura kinachokaa katika moja ya kambi za JWTZ kikikuwa na idadi kubwa ya askari lakini wananchi hawakuwa na taarifa nacho ila kutokana na sababu za kiusalama.

“Unajua kuna kelele za hapa na pale na haya majibizano yanayotokea baina ya Rwanda na Tanzania. Haya ni kama yamewastua watu na kudhani kuwa askari wetu wa Kikosi cha Dharura waliopo hapa Ngara wameletwa maalumu kutokana na tahadhari,” alisema na kufafanua kuwa askari hao wapo siku zote kwa ajili ya kulinda mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kutulia na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Rais Kikwete aliagiza operesheni hiyo ya kuwaondoa wahamiaji haramu ifanyike katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja ikisimamiwa na vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji akiwaonya wahalifu kuwa hapatakuwa na mahali pa kukimbilia wala kujificha.

ROBERT MUGABE NDANI YA IKULU YA ZIMBABWE KWA MARA YA SABA....



Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kinyan’ganyiro cha Urais wa Zimbabwe, Rais Robert Mugabe (89), amefikisha mihula saba ndani ya Ikulu ya nchi hiyo. 

Mugabe juzi alishinda tena kiti cha urais. Matokeo rasmi yalionyesha kuwa aliibuka na ushindi wa asilimia 61 wa kura dhidi ya mpinzani wake, aliyekuwa Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai ambaye alipata asilimia 34.

Chama cha Zanu-PF kinachoongozwa na Mugabe na kile cha MDC cha Tsvangirai, viliunda Serikali ya Muungano mwaka 2008.

Juzi, Tume ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC), ilimtangaza Mugabe kuwa mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika Jumatano iliyopita.

Zanu-PF pia kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa wabunge baada ya kujinyakulia viti 137 kati ya 210.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa hali inaweza kuwa tete hasa baada ya matokeo hayo ambayo yalipingwa na Tsvangirai na chama chake cha MDC. 

Tsvangirai alisema Chama cha MDC kitaisusia Serikali ya Mugabe na kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani. Wasimamizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika wamesema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Aidha, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ilimtaka Tsvangirai akubali matokeo ya uchaguzi.

Wasiwasi

Malalamiko yanayotolewa sasa na wapinzani kuhusu uchaguzi huo yanazidisha uwezekano wa kuibuka machafuko kama yaliyotokea 2008.

  
Mwaka huo, Tsvangirai aliongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais na Zanu-PF kilipinga ushindi huo. Ghasia na machafuko vilitokea na kusababisha kuuawa kwa mamia ya wafuasi wa Tsvangirai.

Umwagaji damu uliotokana na uchaguzi huo ulimfanya Tsvangirai ajitoe kushiriki katika duru ya pili ya uchaguzi na hivyo kutoa mwanya kwa Mugabe kutangazwa kuwa mshindi wa duru hiyo kirahisi.

Hata hivyo, shinikizo la kimataifa lililofuata, lilimlazimu Mugabe kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuishirikisha MDC.

Tayari wananchi wa Zimbabwe katika Mji Mkuu wa Harare wanaamini kwamba wanapaswa kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kujiepusha na kuibuka kwa machafuko.

-Mwananchi.

MSIMAMO WA RAIS KIKWETE KWA RAIS KAGAME WA RWANDA WAUNGWA MKONO KWA ASILIMIA 100 NA WASOMI HAPA NCHINI....



 WASOMI  na  baadhi  ya  wanasiasa  wazalendo nchini wameunga mkono msimamo wa Tanzania uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na chokochoko zinazoanzishwa na Rwanda na wamemtaka Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame, kukaa meza ya mazungumzo na waasi wa nchi hiyo walioko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwani amani haiwezi kutafutwa kwa njia ya mtutu wa bunduki.

Akizungumza na MAJIRA  kwa njia ya simu jana Mhadhiri wa Chuo cha St. Agustino, katika kitivo cha sayansi ya siasa, Prof. Mwesiga Baregu, alisema ushauri alioutoa Rais Kikwete kwa Rais Kagame ni mzuri, hauwezi kuleta athari zozote tofauti na kutumia mtutu wa bunduki kukabili waasi.

"Mimi nikiwa kama mtaalam wa kutatua migogoro suala la mazungumzo ni njia moja ambayo huwa inatumika mara kwa mara na inasaidia kuleta amani," alisema na kuongeza;


"Kutumia mtutu wa bunduki haileti tija kwa mataifa yote mawawili, hivyo ni busara itumike njia ya mazungumzo."


Alitoa mwito kwa nchi jirani kushirikiana kutatua mgogoro uliopo kwa njia ya mazungumzo baina ya Rwanda na DRC.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo cha Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Kitila Mkumbo, alisema anakubaliana na kauli ya Rais Kikwete na anashangazwa na Rais Kagame ni kwa nini anachukizwa kuambiwa azungumze na waasi.

"Maana yake inaonekana hataki kushauriwa...ushauri huo ni kitu kizuri kinaweza kuleta maelewano," alisema Dkt. Mkumbo. Alisema Rais Kagame, anaonekana kama dikteta kutokana na kukataa kuambiwa ukweli na viongozi wenzake.

Alisema kauli ya Rais Kikwete, aliyoitoa kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa saba hakugusia masuala ya vita na anaamini kwamba kwa karne hii sio mwafaka nchi kuingia kwenye vita kwani nchi zina matatizo mengi ambayo yanahitajika kupatiwa ufumbuzi.

"Alichoongea Rais Kikwete, ni msimamo unaotakiwa kuungwa mkono na Watanzania kwani yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na hiyo ndiyo kauli ya nchi...hivyo alichosema ni sawa," alisema Dkt. Mkumbo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alisema ameridhishwa na kauli ya Rais Kikwete, kwani ametumia lugha sahihi katika kueleza hali halisi, hivyo Watanzania wote wanatakiwa kumuunga mkono.

Alisema kwa hali ilivyo ni lazima Watanzania waungane katika masuala kama hayo ili kuleta mshikamano wa nchi.


Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustino Mrema, alisema anamuunga mkono Rais Kikwete, kwa kauli yake hiyo.

Alisema Rais Kagame ameanza chokochoko dhidi ya Tanzania na kwamba hivyo, ndivyo alivyoanza hata Idd Amin. "Siungi mkono vita vitokee, lakini kama atatuchokoza basi tuwe wa mwisho kujibu mapigo," alisema Mrema.

 Aliyekuwa Mhadhiri UDSM, Dkt. Azaveri Lweitama, amezitaka nchi za Afrika Mashariki kukaa chini ili kuangalia jinsi ya kutatua mgogoro huo.

Alisema kuipiga Rwanda ni kazi ndogo sana, lakini hauwezi kumaliza tatizo kwa kutumia bunduki na badala yake ni vyema nchi hizo zikaangalia namna ya kumaliza mgogoro.

"Unajua mnaweza kuingia katika vita mkamuondoa Rias wa Rwanda, lakini bado mkatengeneza matatizo mengine kwa rais ajaye," alisema.

Alisema Kongo kuna waasi wa Rwanda na hata Rwanda pia kuna waasi wa kutoka Kongo, hivyo ni lazima kutafuta njia nzuri ya kutatua tatizo hilo.

Kwa upande mwingine, Dkt. Lweitama, alivitaka vyombo vya habari kutopotosha taarifa zinazozungumzia vita vikitokea hakuna mtu atakayebaki salama.

"Vyombo vya habari vijitahidi kuandika habari zisizo za uchochoezi, kwani hata ninyi pia ni Watanzania, naamini vita ikitokea hakuna mhariri wala mwandishi atakayebaki salama," alisema.

Alisema vyombo vya habari pia vina nafasi ya kukaa chini na kutafakari namna ya kumaliza mgogoro kwa kuwa vina nafasi kubwa kwa mustakabali wa taifa.

Uhusiano wa Tanzania na Rwanda unaelekea kupata mtikisiko baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao.


 Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa nia njema kwa kuwa bado anaamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.

Ushauri ule aliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. ambapo katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli hiyo.

Tangu atoe ushauri huo viongozi wa Rwanga wamekuwa wakitoa kauli za kejeli dhidi ya Tanzania na Rais Jakaya Kikwete. Katika hotuba yake Rais Kikwete, alisema uhusiano wa Tanzania na Rwanda unapitia katika kipindi kigumu

-MAJIRA.

Saturday, 3 August 2013

MREMBO SHINDANO LA MISS AFRICA AUAWA KWA KUCHOMWA VISU.


Mrembo chipukizi amekutwa amekufa kwa kuchomwa kwa visu huku binti yake wa miaka mitatu 'akilia pembeni yake kwenye dimbwi la damu', wamesema marafiki jana.

Mwili wa Linah Keza, mwenye miaka 29, ambaye inafahamika alishiriki kwenye Shindano la Miss Africa 2010, ulikutwa kwenye ghorofa moja huko King Edward Road, Leyton, juzi mapema asubuhi.
Tukio hilo liliripotiwa kwenye Tume Huru ya Polisi ya Malalamiko, ambayo itatazama mawasiliano yake waliyokuwanayo polisi na mwanaume mwenye miaka 38 ambaye amekamatwa kuhusiana na kifo chake.
Madaktari wa Huduma za Gari la Wagonjwa London waliongozana na polisi kwenda mahali hapo kabla ya Saa 10:30 alfajiri, lakini Linah, raia wa Rwanda anayeishi London, alikuwa ameshatangazwa kufariki eneo la tukio.
Inafahamika kwamba binti yake alikuwa mahali hapo wakati wa shambulio hilo, kwa mujibu wa fafiki mmoja wa familia hiyo.
Herbert Muhire alisema: "Binti (yake) amepelekwa kwenye uangalizi na kupatiwa tiba ya kisaikolojia na matukio mengine baada ya kukutwa akilia kando ya mama yake huyo aliyekuwa amelala kwenye dimbwi la damu.
"Familia na marafiki wameelezewa jinsi alivyokuwa ameuawa na kufa kifo cha kutisha.
Rambirambi kwa Linah kutoka kwa marafiki na jamaa ziliachwa kwenye ukurasa wa Facebook uliofunguliwa mara baada ya kifo chake.
Azun Jezan aliandika: "Huzuni mno, roho yake ilale mahali pema peponi na binti yake na familia wajazwe nguvu katika wakati huu mgumu wa huzuni."
Mwingine, Justine Twongyeirwe, aliandika: "Nitakumbuka tabasamu lako mpenzi Linah. Ulale Mahali Pema."
Jana asubuhi, ukurasa huo ulikuwa na wafuasi zaidi ya 500 na baadhi walituma picha za Linah, ambaye alifanya kazi kama mrembo na kusomea huduma za jamii kwenye Chuo Kikuu cha Wolverhampton.
Kwa mujibu wa polisi, mwanaume huyo mwenye miaka 38 alikamatwa baada ya kujisalimisha mwenyewe kwenye kituo cha polisi cha north London juzi.
Msemaji wa polisi alisema: "Uchunguzi wa mauaji umeanza baada ya mwanamke huyo kushambuliwa huko Leyton.
"Polisi waliitwa na Huduma za Gari la Wagonjwa London majira ya Saa 10:29 alfajiri ya Jumatano kwa ripoti za kuchomwa kwa visu.
"Maofisa na Huduma za Gari la Wagonjwa walifika na mwanamke huyo mwenye miaka 29 alikuwa ametangazwa kufariki kwenye eneo la tukio."
Uchunguzi wa mwili wake ulipangwa kufanyika majira ya Saa 5 jana asubuhi kwenye Mochari ya Walthamstow.

MBUNGE WA CCM MTWARA AFUTIWA SHITAKA LA UCHOCHEZI



Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara imemfutia shtaka la kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM)Hasnein Murji .



Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo iliposomwa Julai 3, mwaka huu kwa madai ya kuwa hati ya mashtaka ni dhaifu kisheria na haionyeshi ni makosa yapi mtuhumiwa aliyotenda.


Wakili Kibatala alieleza mahakama kuwa kifungu cha 129 na 132 cha sheria ya mwenendo wa makosa jinai ni lazima mshtakiwa aelezwe mashtaka yake wazi wazi yanayomkabili.


Murji alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo akikabiliwa na kesi ya uchochezi anayodaiwa kuifanya Januari 19,mwaka huu katika eneo la Ligula mkoani hapa.


Hakimu Mkazi Mfawidhi Dynes Lyimo alifuta shtaka hilo na kumwachia mshtakiwa huru baada ya kesi hiyo kuahirishwa tangu Julai 3,mwaka huu. 


Wakati huo huo viongozi wa upinzani Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri wamefikishwa mahakamani.

KESI DHIDI YA WAZIRI MKUU HAINA MANTIKI....SIJAONA SEHEMU ALIYOVUNJA SHERIA"...DPP



MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, amesema haoni mantiki yoyote au uhalali wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kumshitaki Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.


Alisema hayo janai wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, baada ya kufungwa kwa mkutano wa siku tatu wa mawakili wa Serikali wafawidhi, wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi vingine vya Polisi Alisema kauli aliyotoa Pinda bungeni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu kuhusu Polisi kutumia nguvu kwa wananchi, ililenga wanaokaidi kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria na si kupiga na kuua kama ilivyotafsiriwa na wengi.
 
“Sijapata taarifa kwa maandishi juu ya azma ya kumshitaki Waziri Mkuu, lakini Pinda hajavunja sheria kwa kauli yake aliyotoa,” alisema.


Alisema kwa jinsi alivyosikia maelezo ya Waziri Mkuu bungeni, kama LHRC wanamshitaki kwa jinai Waziri Mkuu, haoni uhalali wa mashitaka hayo. 


Usahihi wa Pinda Alisema Waziri Mkuu alieleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya mvunja sheria, na kufafanua kuwa Mtanzania yeyote ana haki kwa mujibu wa sheria, lakini pia ana wajibu, ndiyo maana vipo vyombo na kila chombo kimepewa mamlaka na wajibu wa kutekeleza.


Alifafanua, kwamba kilichoongelewa ni dhana ya mkusanyiko ambayo ni haki kwa mujibu wa Katiba, ikiwemo uhuru wa kukutana, kutoa mawazo na kufanya mawasiliano.


Hata hivyo, alikumbusha kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi, inasema ili mkusanyiko ufanyike, lazima taarifa itolewe kwa kiongozi wa Polisi wa eneo husika.
 
Sheria hiyo inasema, kama mkusanyiko una nia ya kutenda kosa na ikafanyika hivyo, kuna chombo kilichopewa dhamana ya kuhakikisha mkusanyiko haramu unatawanyika na sheria hiyo inaruhusu Polisi kutawanya mkusanyiko haramu.


“Unatarajia nini kama kuna watu wanafanya fujo na polisi wana mamlaka ya kuwakamata waliofanya fujo?” Alihoji Feleshi na kuongeza kuwa dhana ya matumizi ya nguvu ni ya kisheria pia.


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, akizungumza kwa simu na gazeti hili, alisema utaratibu wa Polisi kulazimika kutumia nguvu upo. Aliutaja utaratibu huo kwamba unatumika hasa katika mikusanyiko isiyotakiwa, ambapo Polisi hulazimika kutoa tangazo la angalizo mara kadhaa kutaka watu watawanyike.

“Tangazo linapotolewa, Polisi kwa kutumia kipaza sauti husema, tawanyikeni, tawanyikeni na kusisitiza hivyo mara kadhaa, hapo wanaopaswa kutawanyika wakikaidi, nguvu hutumika ingawa inaweza isiwe ya kupiga risasi, pengine virungu, yote hiyo si kupiga?

“Risasi ni kitu cha mwisho, labda uwe unashambuliwa wewe (polisi), hata ikiwa hivyo, ukipiga risasi kuna maeneo ya kupiga, si kichwani, polisi wana mafunzo ya kupiga maeneo ya miguuni, hivyo kutumia nguvu kwa polisi kupo,” alisema Jaji Werema.

RAIS KIKWETE AMJIBU KAGAME KATIKA HOTUBA YEKE YA MWISHO WA MWEZI JULY



Hii  ni  sehemu  ya  hotuba  yake  ambapo  mheshimiwa Rais  amezungumzia  uhusiano  wa  Tanzania  na  Rwanda.....

Hotuba  kamili  imepachikwa  hapo  chini  baada  ya  nukuu hii.


--------------
Uhusiano na Nchi ya Rwanda

Ndugu wananchi;

Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo. 



Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila mmoja anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.

Napenda kusisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.

Ndugu Wananchi;

Ukweli ni kwamba wakati wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu. 



Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu.
 Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. 


Sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yo yote. Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo. Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right”.

Ndugu Wananchi;

Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi. Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na hata kimataifa. 

 
Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike. 


Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.

Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of context. Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu. 



Tumekuwa tunakutana katika mikutano na vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. 


Wakati wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana ushauri ni wajibu wetu wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu.
 Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo.

Ndugu Wananchi;

Napenda kurudia kusema kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na Rwanda. Tunapenda tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. 



Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu.
 Hatupendi kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.